Uwajibu
wa kuwa na elimu na kuifanyia kazi
Allaamah
swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
Kwa hakika
hakuna budi kwa muislamu kutafuta elimu na kuitendea kazi kwa amali. Na ni
mambo mawili yaendayo sambamba. Kama Alivyosema Allaah (Ta’ala): yeye ndiye Aliyemtuma Mtume Wake kwa
uwongofu na Dini ya Haki. (04:33) “al-Hudaa”
ni elimu yenye manufa. “ad-Diyn-ul-Haqq” ni amali njema. Amali haisihi bila ya
elimu, bali inakuwa ni upotofu. Wala haifai elimu bila ya amali, bali inakuwa
ni hoja dhidi ya mwenye nayo. Ikijumuika elimu na amali – elimu
sahihi na amali njema kwa Muislamu anakuwa katika wale Aliyowaneemesha Allaah; katika
Manabii, masaddiq, mashahidi na watu wema. Na mtu akichukua elimu [tu] akaacha
amali, anakuwa katika wale walioghadhibikiwa [na Allaah]. Nao ni mayahudi na
wanaojifananisha nao. Na mtu akifanya amali tu bila ya elimu, anakuwa katika
waliopotea. Nao ni manaswara na wanaojifananisha nao katika wale wanaomuabudu
Allaah kwa ujinga na upotofu. Na hili
lapatikana mwisho wa suraat-ul-Faatihah. Anasema Allaah(Ta’ala): Tuongoze
katika njia iliyonyooka. Njia ya wale
Uliowaneemesha. (01:06-07) Nao ni
wale walioyajumuisha baina ya elimu yenye manufaa na amali njema. Si(ya
wale) walioghadhibikiwa. (01:07) Nao ni wale waliochukua elimu wakaacha
amali, hivyo wakaghadhibikiwa. Kwa kuwa wamemuasi Allaah kwa
baswiyrah[ujuzi]. Wala waliopotea. (01:07) Nao ni wale waliochukua(fanya) amali bila
ya elimu. Huu ni upotofu na kupinda. Na amali hii haimfai mwenye nayo, bali
inakuwa anajitaabisha na ataulizwa siku ya Qiyaamah. Hivyo ni lazima [mtu] kuwa
na elimu yenye manufaa na amali njema. Na elimu lazima itangulie kabla ya [mtu
kufanya] amali. Ni lazima kwa mtu kusoma vipi atamuabudu Allaah? Vipi
atampwekesha Allaah(‘Azza wa Jalla)?
Vipi ataswali? Vipi atatoa zakaah? Vipi atafunga? Vipi atahiji na kufanya
‘Umrah? Lazima ajifunze kisha ndio alete amali zikifanywa kwa elimu, mpaka ziwe
zimejengeka juu ya msingi sahihi. Akimtakasia Allaah(‘Azza wa Jalla) Anasema Allaah(Ta’ala): basi jua ya kwamba
hapana mungu ila Allaah, na omba maghufira kwa dhambi zako na za Waumini
wanaume na Waumini wanawake. (47:19)
Kaanza kwa elimu kabla ya kauli na amali. Na kaweka imam bukhaariy(Allaah
amrehemu) mlango maalumu kutokana na Aayah hii akauita:
“Mlango
unaozungumzia elimu kabla ya kauli na amali” Amechukua katika Aayah hii. Ni lazima kwa Muislamu asome mambo ambayo
yatamuwezesha kusimama na dini yake; Tawhiyd, ‘Aqiydah, swalah, Zakaah, Swawm,
Hajj na ‘Umrah. Ni lazima kwa kila Muislamu. Haya ni fardhi ’ayn[1] kwa kila muislamu, sawa wanaume na wanawake, mwarabu
na asiyekuwa mwarabu. Ni lazima kuyajua.
Hapewi udhuru yeyote kwa kutoyajua haya.
Na haya ni sahali[kujifunza nayo] – himidi zote ni Zake Allaah. Maulamaa
wamefanya risalah za mukhtasari zilizowazi. Mtu anaweza kujifunza nayo kwa nusu
saa au dakika kama kumi akastafidi, vipi
atamuabudu Mola wake(‘azza wa jalla). Hali kadhalika asome elimu kwa
wanachuoni, asome elimu kwa wanachuoni.
Asitosheke na kusoma [vitabu na mikanda tu], bali asome kwa wanachuoni ima
madrasah au sehemu za majlisi za dhikr kwa Mashaykh wanaofunza katika misikiti.
Hali kadhalika asikilize mihadhara, wito wa kielimu, khutbah ya ijumaa,
barnamiji zinazorushwa kwenye vyombo vya habari katika idhaa ya Qur-aan Tukufu
–kuna barnamiji za kielimu zenye kunufaisha. Anufaike nazo mtu. Baada ya
kusomwa Qur-aan kunakuja barnamiji za kielimu. Elimu inakukuta kila mahala na
wewe uko kwenye kitanda chako, kwenye gari yako nakadhalika; unafungua idhaa
unasikiliiza. Hii ni heri nyingi. Hali kadhalika katika mambo utayostafidi
kwayo ni kuuliza wanachuoni. Anasema Allaah(Ta’ala); basi waulizeni wenye
ukumbusho kama nyinyi hamjui. (16:43) Unapotatizika na jambo, uliza wanachuoni
wakubainishie kinachokutatiza. Njia nyingi ni sahali –himidi zote ni zake
Allaah. Kasema Mtume (swalla
Allaahu ‘alayhi wa sallam): “Mwenye kuchukua njia anatafuta humo elimu, Allaah
Humsahilishia kwayo njia ya kwenda peponi.” Vikao vya dhikr katika misikiti au madrasah,
zote hizo ni khair- himidi zote ni zake Allaah. Lakini tatizo ni kwa Yule
asiyetaka kusoma na akabaki katika ujinga wake. Hasomi wala hastafidi.
Na huenda akafanya ‘ibaadah kwa mfumo usiyo sahihi ilihali naye hajui. Hii ndio
natija ya kutosoma na kustafidi. Yeye ndiye kaipotoa nafasi yake na kapoteza
wakati wake. La sivyo elimu ni sahali -
himidi zote ni zake Allaah. Si lazima uwe
mwanachuoni kigogo. Yatosheleza ukajifunza mambo ya dini yako, na zaidi
ya hapo ni khayr; Katika mambo ya mu’amalat, mirathi,auqaf,wasia na mambo
mengine wanayoyahitajia watu. Haya ukiweza jifunze nayo ustafidi na unufaishe
pia wengine hii ni khayr. lakini aina ya
kwanza mambo ya ‘ibaadah [fardhu ‘ayn] haya hapewi udhuru yeyote kwa kutoyajua.
Ninamuomba Allaah Atuwafikishe sote kwa kauli njema na amali.
Muhadhara
huu unapatikana kwa njia ya sauti katika link hii hapa chini http://www.youtube.com/watch?v=XHrFlsa2D0s
Swalah na salaam zimuendee Mtume wetu Muhammad(swalla
Allaahu ‘alayhi wa sallam) na ahli zake na maswahaba zake
na atakayemfuata kwa wema