image

image

Thursday, November 21, 2013

Salafiyyah Uhakika Wake Na Sifa Zake


السلفية حقيقتها وسماتها
Salafiyyah Uhakika Wake Na Sifa Zake

(2012-05-4/1433-6-13)

´Allaamah Swaalih bin ´Abdillaah bin Fawzaan al-Fawzaan
(Hafidhwahu Allaah)

Mfasiri:
Abu Bakr Khatwiyb al-Atrush
©

بسم الله الرحمن الرحي

Bismillaahi Rahmaani Rahiym. Alhamdulillaahi Rabil-´Aalamiyn. Swalah na salaam zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ahli zake na Maswahaba zake (radhiya Allaahu ´anhum) wote. Amma ba´ad:

Hakika Mtume (swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katueleza kuwa kutatokea mgawanyiko katika Ummah huu kama ilivyotokea katika Ummah zilizotangulia. Na katuusia wakati huo kushikamana na aliokuwemo yeye (swalla Allaahu ´alyhi wa sallam) na Maswahaba wake (radhiya Allaahu ´anhum).
"Wamegawanyika Mayahudi katika mapote 71, wakagawanyika Wakristo katika mapote 72 na Ummah wangu utagawanyika mapote 73. Yote hayo yataingia motoni ila moja tu)) Maswahaba waliuliza: Ni lipi hilo, ewe Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wa Allaah! Akasema: ((Ni lile nililokuwemo mimi na Swahaba zangu." [Ahmad, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na ad-Daarimiy]

"Hakika atakayeishi katika nyinyi ataona khitilafu nyingi, basi jilazimisheni kufuata Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa walioongoka, yashikeni kwa magego mambo yao." [Abu Daawuud, Ahmad, at-Tirmidhiy, Ibn Maajah na ad-Daarimiy]

"Na jiepusheni na mambo ya kuzua, hakika kila kitachozushwa ni bid´ah na kila bid´ah ni upotofu - [katika upokezi mwingine] - na kila upotofu ni Motoni."
Namna hii katuusia Mtume (swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kushikamana na aliokuwemo yeye na Maswahaba wake wakati kutatokea mgawanyiko.


Kwa kuwa ni lazima mgawanyiko utokee na umetokea kama alivyotueleza Mtume (´alayhis-Salaam). Njia ya kuokoka ni kushikama na aliokuwemo Mtume (´alayhis-Salaam) na Maswahaba wake. Hili kundi ndo "Firqatun-Naajiyah" [Kundi Lililookoka] na moto. Makundi mengine yote yataingia Motoni. Hivyo ndo maana ikikaitwa Firqatun-Naajiyah [Kundi Lililookoka], Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Hili ndo kundi linalotofautiana na mengine kwa kufuata kwao Qur-aan na Sunnah. Na yanayoenda kinyume nalo, basi ni kundi potofu hata kama litajinasibisha na Ummah huu. Na mfumo wake unakhalifu mfumo wa Mtume (swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahaba wake. Njia iko wazi - Alhamduli Allaah - ni kufuata Qur-aan na Sunnah na waliokuwemo Salaf wa Ummah huu katika Maswahaba, Taabi´iyn na waliokuja baada ya Taabi´iyn mpaka mwisho wa karne bora, karne ya tatu au ya nne. Kama alivyosema Mtume (swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

 "Karne bora ni yangu, kisha itayofuatia kisha itayofuatia."

[Anasema mpokezi wa Hadiyth hii, sikumbuki alisema karne mbili au tatu].

Baada ya karne bora ndo kutapitika mambo haya [yaani fitina, mgawanyiko nk]. Lakini atayepita katika manhaj ya karne bora hata kama yu katika karne ya mwisho ya dunia ataokoka na kusalimika na Moto.

وَالسَّابِقُونَ الأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللّهُ عَنْهُمْ وَرَضُواْ عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ذَلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ
Na wale waliotangulia awali (katika Uislamu) miongoni mwa Muhaajiriyn (waliohajiri kutoka Makkah), na Answaar (waliowasaida na kuwanusuru Muhaajiriyn katika wakaazi wa Madiynah), na wale waliowafuata kwa ihsaan; Allaah Ameridhika nao, nao wameridhika Naye.  Na Amewaandalia Mabustani yapitayo chini yake mito, watadumu huko (Peponi) milele. Huko ndiko kufuzu kukuu. (09:100)

Allaah Katoa dhamana kwa ataefuata Muhaajiruun na Answaar kwa wema - kwa sharti hii "Ihsaan" [wema]. Si mtu kujiita au kujinasibisha tu bila ya ukweli, ima kwa ujinga au matamanio. Si kila mwenye kujinasibisha na Salaf anakuwa Salafiy, mpaka awe anawafuata kwa wema. Hii ni sharti iliyoweka na Allaah (´Azza wa Jalla).
Na hii inatakikana kwa wafuasi wake kusoma manhaj Salaf, waijue, washikamane nayo bara bara. Ama kujinasibisha nayo tu na mtu huyo hajui manhaj yao wala madhehebu yao, huyu hatopata kitu wala kumfaa kituNa si katika Salaf [wema waliotangulia] na wala si Salafiyyah. Kwa kuwa hakuwafuata Salaf kwa wema kama Alivyoshurutisha Allaah (´Azza wa Jalla). Nyinyi katika chuokikuu hichi, na katika mji huu na katika misikiti ya mji huu kinachofunzwa ni manhaj Salaf-us-Swaalih. Mpaka tuwafuate kwa wema si kwa kudai tu au kujiita.
Ni wangapi wamedai kuwa Salafiyyah na wamedai kuwa wako katika manhaj Salaf nao wako kinyume na hilo. Ima kwa kutokujua manhaj Salaf au kwa matamanio. Anajua lakini anafuata matamanio yake na wala hafuati manhaj ya Salaf. Khasa kwa yule anayepita katika manhaj Salaf kunahitajika mambo mawili kama tulivyosema, jambo la kwanza ni kujua kwanza manhaj [mfumo/njia] ya Salaf. Jambo la pili kushikamana nayo bila kujali shida utazopata. Kwa kuwa kutajitokeza wenye kuikhalifu [kwenda kinyume nayo/kuipinga] maudhi, matusi, majina ya kejeli nk. Lakini kuwa na subira kwa hayo kwa kuwa amepewa mtihani katika yale aliomo, asibabaike. Asubiri kwa hayo mpaka atapokutana na Mola Wake. Asome manhaj  Salaf kwanza, awafuate kwa wema, asubiri kwa [mitihani] itayompata kutoka kwa watu. Hayatoshi haya, ni lazima kuyaeneza madhehebu ya Salaf, ni lazima afanye Da´wah kwa njia ya Allaah, alinganie manhaj Salaf, awabainishie watu, ayaeneze kwa watu. Huyu ndiye Salafiy hakika [wa kweli]. Ama mwenye kudai Salafiyyah naye hajui manhaj Salaf, au anajua na hawafuati bali yeye anafuata yale waliomo watu, au anafuata yale yalioafikiana na matamanio yake. Huyu si Salafiyyah hata akijiita Salafiy - au asisubirie fitina [mitihani] na akawa anapakana mafuta katika dini yake, kupakana mafuta kwa chochote katika manhaj Salaf. Huyu si katika manhaj Salaf. ´Ibra si kujiita, ´ibra ni uhakika.


Hivyo yatakikana kwetu kujua manhaj Salaf na kusoma manhaj Salaf katika ´Aqiydah, tabia, kazi. Katika mambo yote. Kwa kuwa ndo manhaj aliokuwemo Mtume wa Allaah (swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahaba wake katika Muhaajiruun na Answaar (radhiya Allaahu ´anhum) na waliowafuata mpaka kitaposimama Qiyaamah. Kasema Mtume (swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

"Hakitoacha kikundi katika Ummah wangu... "

Hawa ndo Salafiyyuun.   

"Hakitoacha kikundi katika Ummah wangu kuwa juu ya haki dhahiri, hawatowadhuru wataowalaumu wala kwenda kinyume nao mpaka ifike amri ya Allaah (yaani kifike Qiyaamah).”

Kauli ya yake "Hawatowadhuru wataowalaumu wala wenye kwenda kinyume nao" ni dalili ya kuonesha kutakuwa wenye kwenda kinyume nao na wenye kuwalaumu, lakini hilo halitowababaisha. Bali atachukua njia yake ya kumfikisha kwa Allaah (´Azza wa Jalla) na asubiri kwa yatayomfika. Kama alivyosema Luqmaan kwa mwanawe ilihali ni mwenye kumpa nasaha:

يَا بُنَيَّ أَقِمِ الصَّلَاةَ وَأْمُرْ بِالْمَعْرُوفِ وَانْهَ عَنِ الْمُنكَرِ وَاصْبِرْ عَلَى مَا أَصَابَكَ إِنَّ ذَلِكَ مِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ وَلَا تُصَعِّرْ خَدَّكَ لِلنَّاسِ وَلَا تَمْشِ فِي الْأَرْضِ مَرَحًا إِنَّ اللَّهَ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ وَاقْصِدْ فِي مَشْيِكَ وَاغْضُضْ مِن صَوْتِكَ إِنَّ أَنكَرَ الْأَصْوَاتِ لَصَوْتُ الْحَمِيرِ
“Ewe mwanangu! Shika Swalah, na amrisha mema, na kataza maovu, na subiri kwa yanayokupata. Hayo ni katika mambo ya kuazimiwa. Wala usiwabeuwe watu, wala usitembee katika ardhi kwa maringo. Hakika Allaah Hampendi kila anayejivuna na kujifakhirisha. Na ushike mwendo wa katikati, na teremsha sauti yako. Hakika katika sauti mbaya zote bila ya shaka iliyozidi ni sauti ya punda.” (31:17-19)

Hii ndo manhaj Salaf! Hizi ni sifa zao!

وَأَنَّ هَـذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ وَلاَ تَتَّبِعُواْ السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ذَلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Na kwamba hii Njia Yangu iliyonyooka, basi ifuateni. Na wala msifuate vijia (vinginevyo) vitakufarikisheni na Njia Yake. Hivyo ndivyo Alivyokuusieni (Allaah) kwayo mpate kuwa na taqwa.” (06:153)
"Hii ndio Njia Yangu", kainasibisha Kwake. Unasibisho wa kukazia - kwake na kwa mwenye kuipita.”

وَأَنَّ هَـذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ وَلاَ تَتَّبِعُواْ السُّبُلَ
“Na kwamba hii Njia Yangu iliyonyooka, basi ifuateni. Na wala msifuate vijia (vinginevyo)” (06:153)

Ni dalili ya kuonesha kuwa kuna vijia vinginevyo, wala hakuziwekea mpaka ni njia nyingi.

وَلاَ تَتَّبِعُواْ السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ

“Wala msifuate vijia vinginevyo,vitakufarikisheni na Njia Yake. ” (06:153)
Huu ndo mfumo wa mapote yanayokhalifu manhaj Salaf. 

وَلاَ تَتَّبِعُواْ السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ذَلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Na wala msifuate vijia (vinginevyo) vitakufarikisheni na Njia Yake. Hivyo ndivyo Alivyokuusieni (Allaah) kwayo mpate kuwa na taqwa.” (06:153)

Jambo la kwanza Kasema "Ifuateni", kisha akasema "Amekuusieni", akikazia.

ذَلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Hivyo ndivyo Alivyokuusieni (Allaah) kwayo mpate kuwa na taqwa (kumcha).” (06:153)

Kumcha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na kuogopa upotofu na kuogopa utata na kuogopa yanayokwenda kinyume na njia yenu katika kupita kwenu katika Njia hii. Ni dalili kuonesha kuwa  mtafikwa na mambo, na angalia Alivyoifanya Njia Yake kuwa moja na Akavifanya vijia vinginevyo kuwa vingi. Njia ya Allaah ni moja haikupinda wala si nyingi wala haiendi kinyume, ama vijia vinginevyo ni vingi. Kila [pote] mtu amechukua njia yake aipitayo, kila [pote] mtu amechukua mfumo wake aupitao yeye na wafuasi wake. Vijia vinginevyo ni vingi.

وَلاَ تَتَّبِعُواْ السُّبُلَ

“Na wala msifuate vijia (vinginevyo).” (06:153)

Ukipita njia nyingine, itakuwa vipi?

فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ

”Vitakufarikisheni na Njia Yake.” (06:153)


Itawatoa katika Njia ya Allaah (´Azza wa Jalla). Mtatumbukia katika upotofu na maangamivu. Hivyo hakuna kuokoka, wema wala mafanikio ila kwa kushikamana na Njia iliyonyooka. Ambayo ndio Njia ya Allaah (´Azza wa
Jalla). Na kila yenye kwenda kinyume nayo ni njia ya Shaytwaan, katika kila njia katika hizo kuna Shaytwaan anaelingania watu kwazo. Tuwe tahadhari na jambo hili. Na tusidanganyike na wengi wenye kuikhalifu, utata wao na kutuponda kwao. Tusijali! Bali twenda kwa Allaah kwa baswiyrah [elimu]. Allaah (Jalla wa ´Alaa) Katufaradhisha juu yetu katika kila swalah kusoma suurat-ul-Faatihah. Na mwisho wake [Kasema]:

اهدِنَــــا الصِّرَاطَ المُستَقِيمَ

“Tuongoe Njia iliyonyooka.” (01:06)

Njia ambayo ndio ya Allaah (Jalla wa ´Alaa).

وَأَنَّ هَـذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا

 “Na kwa hakika hii ndiyo Njia yangu Iliyo Nyooka.” (06:153)

اهدِنَــــا الصِّرَاطَ المُستَقِيمَ

“Tuongoe njia iliyonyooka.” (01:06)

Yaani tuongoze na utuelekeze na ututhibitishie katika Njia iliyonyooka.


صِرَاطَ الَّذِينَ أَنعَمتَ عَلَيهِمْ

“Njia ya uliowaneemesha.” (01:07)

Ni kina nani wanaopita katika Njia hio? Ambao Allaah Amewaneemesha katika Manabii, Massiddiqi, Mashahidi, Watu wema, na uzuri ulioje kuwa pamoja na watu hao! Watu hawa ndio viongozi katika Njia hii unayopita wewe.

وَمَن يُطِعِ اللّهَ وَالرَّسُولَ فَأُوْلَـئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللّهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاء وَالصَّالِحِينَ وَحَسُنَ أُولَـئِكَ رَفِيقًا

“Na wenye kumtii Allaah na Mtume, hao wapamoja na wale alio waneemesha Allaah miongoni mwa Manabii, na Masiddiqi, na Mashahidi, na Watu wema. Na uzuri ulioje kuwa pamoja na watu hao!” (04:69)

Usibabaike na wewe uko katika Njia hii. Kwa kuwa wenzako na viongozi wake ni watu Bora zaidi. Usibabaike hata kama njia zimekuwa nyingi leo, mapote yamekuwa mengi, wamekuwa wengi wenye kwenda kinyume nayo, usijali. Kwa kuwa wewe umepewa mtihani katika uliomo, nayo ni Njia ya Allaah (´Azza wa Jalla).

غَيرِ المَغضُوبِ عَلَيهِمْ وَلاَ الضَّالِّينَ

“Siyo ya walio kasirikiwa, wala waliopotea.” (01:07)


Yaani sio Njia ya walio kasirikiwa, wala waliopotea. Walio kasirikiwa ni wale wenye elimu na hawakuifanyia kazi, kama mayahudi. Wana elimu lakini hawakuifanyia kazi. Na elimu kama haikufanyiwa kazi inakuwa ni hoja dhidi ya mwenye nayo siku ya Qiyaamah. Na elimu ikiwa ni maneno tu bila ya matendo itampeleka mwenye nayo Motoni. Ni lazima matendo. Na elimu bila ya matendo ni kama mti bila ya matunda. Una faida gani mti huyu, mti bila ya matunda? Hivyo ndo maana Allaah Amewakasirikia. Kwakuwa wako na elimu na hawakuifanyia kazi, wakastahiki ghadhabu za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hata kama wataona wao ndo watu bora, waliombele, watu wa ruqyah na mengineyo wanayodai kunako Ruqyah. Wamo katika upotofu! Wamo katika khasira za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

غَيرِ المَغضُوبِ عَلَيهِمْ وَلاَ الضَّالِّينَ

“Siyo ya waliokasirikiwa, wala waliopotea.”(01:07)

Yaani sio njia ya waliopotea. Nao ni wale wenye kufanya kazi [kutenda], wanamuabudu Allaah, wanajitahidi nk lakini bila ya elimu na uongofu kutoka kwa Allaah (Subhaaanahu wa Ta´ala). Matendo yao ni bure hayatowafaa kitu. Kwa kuwa wao wamepotea katika Njia, wamepotea katika Njia iliyonyooka. Matendo yao ni kuchoka bila ya faida. Miongoni mwa watu hawa ni manaswara. Wana ´ibaadah, upole nk lakini wanafanya bila ya elimu. Wamepotea! Wako makosani! ´Ibra sio kujitahidi bila ya kuisibu haki, kinyume na Njia sahihi.

Kwa mfano Masufi wenzetu katika Uislamu wamo katika njia ya manaswara. Wanamuabudu Allaah, wanaipa nyongo dunia, wanajitahidi nk lakini hawana elimu. Na hawasomi, wanaisusa elimu. Wanawaambia watu fanye amali, vipi elimu itawakosesha kufanya amali. Kinachohitajika kwenu ni matendo. Wanataka kuwatoa watu katika elimu, kukaa na wanachuoni, kuchukua elimu kwa wanachuoni. Wanasema watu hawa ni wapungufu wako hivi na vile, vipi mnakosa kufanya amali! Hili ni jambo la kwanza.

Jambo la pili wanasema elimu haiji kwa kusoma, elimu inakuja hivi tu! Utapojishughulisha na ´ibaadah Allaah Atakupa elimu bila hata ya kusoma. Huu ni upotofu - A´udhubi Allaah.
Tuwe tahadhari na hili, elimu inakuja kwa kusoma. Huwezi kuifikia elimu ila kwa kusoma kwa wanachuoni. Elimu inatangulia kabla ya kauli na amali. Kasema Imaam Bukhaariy (rahimahu Allaah) katika swahiyh Bukhaariy: Mlango "Elimu kwanza kabla ya kauli na amali."
Kisha akataja Aayah hii:

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ

“Basi jua ya kwamba hapana mungu wa haki ila Allaah, na omba maghufira kwa dhambi zako na za Waumini wanaume na Waumini wanawake.” (47:19)

Jua kwanza ya kwamba hapana mungu wa haki ila Allaah, soma kwanza kisha ndo uombe maghufira na ufanya amali baada ya kujua. Ni lazima mtu kusoma, elimu ndo dalili kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´a). Allaah Kateremsha Kitabu na Katuma Mtume ili atuelekeze katika Njia sahihi ambayo tutapita kwayo - nayo ni elimu yenye manufaa na amali njema. Allaah (Jalla wa ´Alaa) Kasema:
 
هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَى وَدِينِ الْحَقِّ

“Yeye Ndiye aliyemtuma Mtume Wake kwa uongofu na Dini ya Haki.” (09:33)
Uongofu ni elimu yenye manufaa, na dini ya haki ni amali njema. Lazima mtu akusanyike mambo mawili, elimu yenye manufaa na amali njema. Hayo ndo aliokuja nayo Mtume (swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakuja na elimu tu bila ya amali, na wala hakuja na amali tu bila ya elimu. Mambo mawili lazima yende sambamba.

Lazima amali [za kila mtu] ziwe zimejengeka juu ya elimu na baswiyrah. Na ni lazima kwa mwanachuoni aifanyiekazi elimu yake la sivyo mwanachuoni asiyeifanyia kazi elimu yake na mtendaji asiyepita katika elimu, wote wawili wameangamia. Isipokuwa tu yule mwenye elimu yenye manufaa na amali njema. Na hili ndo alilotumwa nalo Mtume (swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).
Huu ndo u-Salafiyyah wa kihakika, na hizi ndo sifa za Salaf-us-Swaalih [wema waliotangulia]. Elimu yenye manufaa na amali njema. Hizi ndo sifa za Salaf-us-Swaalih. Salaf ni wale waliotangulia.
وَالَّذِينَ جَاؤُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَؤُوفٌ رَّحِيمٌ

“Na waliokuja baada yao wanasema: Mola Wetu! Tughufirie sisi na ndugu zetu walio tutangulia kwa Iymaan.” (59:10)

Alipotaja Muhaajiruun na Answaar katika Suurat al-Hashr. Akasema [Allaah]:

وَالَّذِينَ جَاؤُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَؤُوفٌ رَّحِيمٌ

“Na waliokuja baada yao wanasema: Mola Wetu! Tughufirie sisi na NDUGU zetu walio tutangulia kwa Iymaan, wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu undani [chuki] kwa walioamini. Mola Wetu! Hakika Wewe ni Mpole na Mwenye kurehemu.” (59:10)
Anaewachukia waliotangulia miongoni mwa Maswahaba katika Muhaajiruun na Answaar - karne bora, yule anaewachukia huenda Allaah Akamkasirikia na kumghadhibikia na amali zake zikawa bure bila ya malipo.
Kwa kuwa [amali zake] hazikujengeka katika uongofu. Na amali [matendo] yanakubaliwa kwa sharti mbili.

Sharti ya kwanza amali hizo ziwe khalisi kutafuta Uso [Pepo] ya Allaah. Sharti ya pili ziwe zinaenda sambamba na Sunnah za Mtume wa Allaah.
بَلَى مَنْ أَسْلَمَ وَجْهَهُ لِلّهِ وَهُوَ مُحْسِنٌ

“Sivyo hivyo! Yeyote anaye elekeza uso wake kwa Allaah naye ni mtenda mema.” (02:112)

Kauelekeza uso wake kwa Allaah, hii ndio Ikhlaasw. Kujiweka mbali kabisa na shirki na washirikina.
وَهُوَ مُحْسِنٌ

“Naye ni mtenda mema.” (02:112)

Yaani anamfuata Mtume (swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kaacha bid´ah na mambo ya kuzusha. Bali anatenda kwa mujibu wa Sunnah za Mtume (swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). 

بَلَى مَنْ أَسْلَمَ وَجْهَهُ لِلّهِ وَهُوَ مُحْسِنٌ فَلَهُ أَجْرُهُ عِندَ رَبِّهِ وَلاَ خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلاَ هُمْ يَحْزَنُونَ
“Sivyo hivyo! Yeyote anaye elekeza uso wake kwa Allaah naye ni mtenda mema, basi ana malipo yake kwa Mola Wake, wala haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.” (02:112)

Hii ndo manhaj Salaf. Nayo imechukuliwa katika Qur-aan na Sunnah. Usiseme wapi tumetoa Manhaj Salaf? Mimi sijui mambo haya ya mfumo wa Salaf, wapi mmetoa haya jamani? Ndugu yangu, ni katika Qur-aan na Sunnah. Qur-aan na Sunnah ndivyo vitavyokufunza Manhaj Salaf. Usichukue katika Qur-aan na Sunnah ila kwa kupitia kwa wanachuoni, waliobobea katika elimu.

Ni jambo la lazima! Yule atakayekupita katika manhaj Salaf lazima ashikamane na dhwawaabit hizi za Kishari´ah. Vinginevyo kuna wengi leo wanaodai wako katika manhaj Salaf, nao wako katika upotofu na makosa makubwa. Wanayanasibisha na manhaj Salaf. Hivyo ikawa makafiri, wanafiki na wale nyoyo zao zina maradhi wakawa wanawatukana Salafiyyuun. Na kila jarima, uharibifu, na kila balaa wakasema "Ni hawa Salafiyyuun ndo wenye kufanya hivi." Haya Salaf imejiweka nayo mbali kabisa na mtu mwenye kufanya hivi si katika manhaj Salaf, bali mtu huyu yu katika mfumo potofu. Hata akidai yu katika manhaj Salaf.

Lazima tutofautishe yule mwenye kujiita hivyo na uhakika, kwa kuwa kuna wanaojiita hivyo bila ya uhakika. Mtu huyu si Salafiyyah, na Salaf wako mbali naye. Manhaj Salaf ni elimu yenye manufaa, amali njema, udugu katika dini ya Allaah, kusaidiana katika wema na ucha Mungu. Hii ndo manhaj Salaf-us-Swaalih. Mfumo ambao mtu akishikamana nao ameokoka na fitina na yuko katika radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

 رَّضِيَ اللّهُ عَنْهُمْ وَرَضُواْ عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ذَلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ
“Allaah Ameridhika nao, na wao wameridhika Naye; na Amewaandalia Bustani zipitazo mito kati yake. (09:100)

Sote tunaitaka Pepo ipitayo mito kati yake. Sote hatutaki Moto wala adhabu. Lakini tunachoongelea ni kutafuta zile sababu zitazotufikisha Peponi na kutuokoa na Moto. Hakuna sababu zaidi ya kushikamana na manhaj Salaf-us-Swaalih. Kasema Imaam Maalik (rahimahu Allaah):
"Hautofaulu mwisho wa Ummah huu ila kwa waliofaulu nayo wa mwanzo wao."
Watu wa mwanzo walifaulu kwa kitu gani? Ilikuwa ni Qur-aan na Sunnah. Vivyo hivyo hautofaulu mwisho wa Ummah huu ila kwa Qur-aan na Sunnah. Na Qur-aan na Sunnah - Alhamduli Allaah, vipo mbele yetu. Vimehifadhiwa na hifdh ya Allaah.

إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ

“Hakika Sisi ndio tulioteremsha Ukumbusho huu (Qur-aan), na hakika Sisi ndio tutaolinda.” (15:09)

Umelindwa kwa idhini ya Allaah. Mwenye kutaka haki na elimu sahihi atapata haya.
Ama mwenye kudai tu bila ya uhakika, au anafuata kichwa mchunga mwenye kudai Salafiyyah na si katika manhaj Salaf huyu hapati kitu. Tatizo watu hawa wanajinasibisha na Salafiyyah, na huu ni uongo mtupu kwa Salaf, uongo mtupu kwa Salafiyyah. Huku ni kukimbiza watu sawa ikiwakakusudia hili au hakukusudia. Itakuwa ima ni jitu lenye matamanio au ni mjinga. Madai yasiyosimamishiwa dalili watu wake ni wenye kudai tu. Ni lazima kwa mwenye kudai na kujinasibisha na Salaf ahakikishe jina hili na unasibisho huu kwa kuonekana kwake kweli manhaj Salaf; sawa katika Itikadi yake, kauli yake, amali zake, matangamano yake mpaka awe Salafiyyah wa haki na awe kiigizo bora.
Mwenye kutaka manhaj hii ni juu yake kuijua, kuisoma, kuifanyia kazi yeye kwanza, awalinganie watu kwayo, awabainishie watu. Hii ndio njia ya kuokoka na hii ndio njia ya Firqat-un-Naajiyah Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wale walioko katika yale aliokuwemo Mtume (swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahaba wake na akawa na subira juu ya hilo, akawa imara kwa hilo, Akawa hatopelekwa na fitina wala na madai potofu bali akawa imara kwa yale aliomo mpaka atapokutana na Mola Wake (Subhaanahu wa Ta´ala).


Swalah na salaam zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ahli zake na Maswahaba zake (radhiya Allaahu ´anhum) wote.

Sunday, June 2, 2013

dharurah ya kuwa na elimu sahihi na amali njema



     Uwajibu wa kuwa na elimu na kuifanyia kazi
Allaamah   swaalih   bin  Fawzaan   al-Fawzaan
Kwa hakika hakuna budi kwa muislamu kutafuta elimu na kuitendea kazi kwa amali. Na ni mambo mawili yaendayo sambamba. Kama Alivyosema Allaah (Ta’ala):  yeye ndiye Aliyemtuma Mtume Wake kwa uwongofu na Dini ya Haki. (04:33)  “al-Hudaa” ni elimu yenye manufa. “ad-Diyn-ul-Haqq” ni amali njema. Amali haisihi bila ya elimu, bali inakuwa ni upotofu. Wala haifai elimu bila ya amali, bali inakuwa ni hoja dhidi ya mwenye nayo. Ikijumuika elimu na amali – elimu sahihi na amali njema kwa Muislamu anakuwa katika wale Aliyowaneemesha Allaah; katika Manabii, masaddiq, mashahidi na watu wema. Na mtu akichukua elimu [tu] akaacha amali, anakuwa katika wale walioghadhibikiwa [na Allaah]. Nao ni mayahudi na wanaojifananisha nao. Na mtu akifanya amali tu bila ya elimu, anakuwa katika waliopotea. Nao ni manaswara na wanaojifananisha nao katika wale wanaomuabudu Allaah kwa ujinga na upotofu. Na hili  lapatikana mwisho wa suraat-ul-Faatihah. Anasema Allaah(Ta’ala): Tuongoze katika  njia iliyonyooka. Njia ya wale Uliowaneemesha. (01:06-07)  Nao ni wale walioyajumuisha baina ya elimu yenye manufaa na amali njema. Si(ya wale)  walioghadhibikiwa. (01:07)  Nao ni wale waliochukua elimu wakaacha amali, hivyo wakaghadhibikiwa. Kwa kuwa wamemuasi Allaah kwa baswiyrah[ujuzi]. Wala waliopotea. (01:07)  Nao ni wale waliochukua(fanya) amali bila ya elimu. Huu ni upotofu na kupinda. Na amali hii haimfai mwenye nayo, bali inakuwa anajitaabisha na ataulizwa siku ya Qiyaamah. Hivyo ni lazima [mtu] kuwa na elimu yenye manufaa na amali njema. Na elimu lazima itangulie kabla ya [mtu kufanya] amali. Ni lazima kwa mtu kusoma vipi atamuabudu Allaah? Vipi atampwekesha Allaah(‘Azza wa Jalla)?  Vipi ataswali? Vipi atatoa zakaah? Vipi atafunga? Vipi atahiji na kufanya ‘Umrah? Lazima ajifunze kisha ndio alete amali zikifanywa kwa elimu, mpaka ziwe zimejengeka juu ya msingi sahihi. Akimtakasia Allaah(‘Azza wa Jalla)  Anasema Allaah(Ta’ala): basi jua ya kwamba hapana mungu ila Allaah, na omba maghufira kwa dhambi zako na za Waumini wanaume na Waumini wanawake. (47:19)
 Kaanza kwa elimu kabla ya kauli na amali. Na kaweka imam bukhaariy(Allaah amrehemu) mlango maalumu kutokana na Aayah hii akauita:
“Mlango unaozungumzia elimu kabla ya kauli na amali” Amechukua katika Aayah hii.   Ni lazima kwa Muislamu asome mambo ambayo yatamuwezesha kusimama na dini yake; Tawhiyd, ‘Aqiydah, swalah, Zakaah, Swawm, Hajj na ‘Umrah. Ni lazima kwa kila Muislamu. Haya ni fardhi ’ayn[1]  kwa kila muislamu, sawa wanaume na wanawake, mwarabu na asiyekuwa mwarabu. Ni lazima kuyajua.  Hapewi udhuru yeyote kwa kutoyajua haya.  Na haya ni sahali[kujifunza nayo] – himidi zote ni Zake Allaah. Maulamaa wamefanya risalah za mukhtasari zilizowazi. Mtu anaweza kujifunza nayo kwa nusu saa au dakika kama kumi akastafidi, vipi  atamuabudu Mola wake(‘azza wa jalla). Hali kadhalika asome elimu kwa wanachuoni, asome  elimu kwa wanachuoni. Asitosheke na kusoma [vitabu na mikanda tu], bali asome kwa wanachuoni ima madrasah au sehemu za majlisi za dhikr kwa Mashaykh wanaofunza katika misikiti. Hali kadhalika asikilize mihadhara, wito wa kielimu, khutbah ya ijumaa, barnamiji zinazorushwa kwenye vyombo vya habari katika idhaa ya Qur-aan Tukufu –kuna barnamiji za kielimu zenye kunufaisha. Anufaike nazo mtu. Baada ya kusomwa Qur-aan kunakuja barnamiji za kielimu. Elimu inakukuta kila mahala na wewe uko kwenye kitanda chako, kwenye gari yako nakadhalika; unafungua idhaa unasikiliiza. Hii ni heri nyingi. Hali kadhalika katika mambo utayostafidi kwayo ni kuuliza wanachuoni. Anasema Allaah(Ta’ala); basi waulizeni wenye ukumbusho kama nyinyi hamjui. (16:43)   Unapotatizika na jambo, uliza wanachuoni wakubainishie kinachokutatiza. Njia nyingi ni sahali –himidi zote ni zake Allaah.  Kasema Mtume (swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam): “Mwenye kuchukua njia anatafuta humo elimu, Allaah Humsahilishia kwayo njia ya kwenda peponi.”  Vikao vya dhikr katika misikiti au madrasah, zote hizo ni khair- himidi zote ni zake Allaah. Lakini tatizo ni kwa Yule asiyetaka kusoma na akabaki katika ujinga wake. Hasomi wala hastafidi. Na huenda akafanya ‘ibaadah kwa mfumo usiyo sahihi ilihali naye hajui. Hii ndio natija ya kutosoma na kustafidi. Yeye ndiye kaipotoa nafasi yake na kapoteza wakati wake. La sivyo elimu ni sahali  - himidi zote ni zake Allaah. Si lazima uwe  mwanachuoni kigogo. Yatosheleza ukajifunza mambo ya dini yako, na zaidi ya hapo ni khayr; Katika mambo ya mu’amalat, mirathi,auqaf,wasia na mambo mengine wanayoyahitajia watu. Haya ukiweza jifunze nayo ustafidi na unufaishe pia wengine hii ni khayr.  lakini aina ya kwanza mambo ya ‘ibaadah [fardhu ‘ayn] haya hapewi udhuru yeyote kwa kutoyajua. Ninamuomba Allaah Atuwafikishe sote kwa kauli njema na amali.
Muhadhara huu unapatikana kwa njia ya sauti katika link hii hapa chini http://www.youtube.com/watch?v=XHrFlsa2D0s
Swalah na salaam zimuendee Mtume wetu Muhammad(swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)  na ahli zake na maswahaba zake na atakayemfuata kwa wema